Vibali vya uchimbaji mchanga vyasitishwa Kinondoni

0
362

Mkuu wa wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es salaam, – Daniel Chongolo amesitisha vibali vya uchimbaji mchanga vilivyotolewa na Bodi ya Maji Bonde la Ruvu kutokana na kusababisha uharibifu wa mito.
 
Vibali vilivyositishwa ni vile vilivyotolewa kufanya shughuli za uchimbaji katika bonde la mto Salasala, mto mbezi, mto Ndumbwi pamoja na mto Nyakasangwe na kusema kuwa mito hiyo inapita katikati ya makazi ya watu na kwamba baada ya kufanyika marekebisho utawekwa utaratibu upya wa kufanya shughuli hizo.
 
Akizungumza  mara baada ya kufanya ziara katika bonde la mto Salasala, – Chongolo amesema kuwa amefikia uamuzi huo baada ya watu waliopewa vibali vya kufanya uchimbaji huo kuendeleza uharibifu.
 
Amesema kuwa kinachofanyika hivi sasa ni kurekebisha mito hiyo kwa kupanda miti, magugu  na mianzi inayoshika ardhi ili kuzuia mmomonyoko wa udongo.
 
Mkuu huyo wa wilaya ya Kinondoni amefafanua kuwa  ameruhusu vibali vya uchimbaji mchanga ndani ya wilaya hiyo kutolewa katika bonde la mto Mpigi kwa maelekezo ya kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa ajili ya kusafisha mto huo.