Rais Dkt. John Magufuli amerejea kuwasisitiza viongozi mbalimbali ambao amekua akiwateua kwenda kuwatumikia wananchi kwa uaminifu na uadilifu.
Akizungumza leo Ikulu jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni, Rais Magufuli amesema kuwa bado wananchi wanawategemea viongozi wao kuwasaidia katika mambo mbalimbali, hivyo ni vyema viongozi hao wakawatumikia kwa uaminifu.
Pia amewataka viongozi hao kushirikiana na watendaji wengine katika sehemu zao za kazi ili kuhakikisha lengo la serikali katika kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi linafikiwa.
Miongoni mwa viongozi walioapishwa ni Brigedia Jenerali Suleiman Mzee anayekua Kamishna Jenerali wa Magereza akichukua nafasi ya Phaustine Kasike ambaye ameteuliwa kuwa Balozi, na Dkt Hassan Abbas anayekua Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo kabla ya uteuzi huo alikua Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali.
Naye John Masunga ameapishwa kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuchukua nafasi ya Thobias Andengenye ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Magufuli.
Hafla ya kuwaapisha viongozi hao imehudhudhuriwa na viongozi waandamizi mbalimbali wakiwemo wa serikali, dini pamoja na wale wa vyombo vya ulinzi na usalama.