Mtume Boniface Mwamposa anashikiliwa na jeshi la polisi kufuatia watu 20 kufariki dunia na 16 kujeruhiwa katika mkutano wake mjini Moshi wakati wakigombea kukanyaga mafuta yanayodaiwa kuwa na upako.
Akizungumzia tukio hilo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema kuwa Mwamposa amekamatiwa jijini Dar es Salaam akitaka kutoroka, na sasa wanafikiria kumrejesha Kilimanjaro ili akawajibike.
“Tunashangaa kweli kwanini alitaka kukimbia. Huyu ni mchungaji anayeombea watu, sasa kwanini wakati watu wamepata matatizo yeye akimbie? Yote haya yatadhihirika huko mbeleni,” amesema Simbachawene.
Aidha, amewataka wale wote wanaotoa huduma kama ya Mwamposa kufahamu kuwa wana wajibu wa kuhakikisha usalama wa watu wanaowakusanya.
Amesema kitendo cha Mwamposa kuwataka watu zaidi ya 10,000 kupita kwenye mlango mmoja ulio mdogo ili kukanyaga mafuta hayo hakikuwa sahihi.
Miili ya waliofariki itaagwa kesho kwenye uwanja huo, ambapo hadi sasa tayari miili 16 ya waliofariki imetambuliwa.