Vifo vya uzazi vyapungua hospitali ya rufaa Mwanza

0
387
Kutoka kushoto: Katibu wa Afya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure, Lilian Munis, Kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali ya Sekou Toure, Dkt Englibert Rauya, na Gerald Chami, mkuu wa kitengo cha mawasiliano Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika kampeni ya 'tunaboresha sekta ya afya.'

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure, imepunguza vifo vitokanavyo na uzazi baada ya kuboreshwa kwa huduma za uzazi hospitalini hapo.

Akizungumza jijini Mwanza wakati wa kampeni ya ‘Tunaboresha sekta ya afya’ inayoendeshwa na maofisa habari wa taasisi zilizoko chini ya wizara ya afya, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Uzazi na Vizazi, Clement Morabu, amesema hospitali hiyo inatoa huduma ya uzazi kwa kina mama 700 kwa mwezi.

“Idadi ya wanawake wanaojifungua imeongezeka, miaka ya nyuma ilikuwa chini ya 500 kwa mwezi, lakini sasa ni 700 kwa mwezi.

“Pia vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua. Mwaka 2017 vifo vilikuwa 21, mwaka 2018 vilikuwa 14 na mwaka 2019 ni 10. Mpango wetu ni kutokomeza kabisa vifo vitokanavyo na uzazi,” amesema Morabu.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dkt. Engelbert Rauya amesema wameanza ujenzi wa jengo la mama na mtoto lenye urefu wa ghorofa tano.

“Jengo hilo mpaka sasa limeshatumia Sh bilioni 4 na tunatarajia kutumia Tsh bilioni 10.

“Kwa sasa hospitali inatumia vitanda 315 ambavyo havitoshi, lakini jengo hili litakuwa na vitanda 565. Hii itasaidia kupunguza msongamano na pia idadi ya kina mama itaongezeka” amebainisha Dkt. Rauya.

Ujenzi wa jengo jipya unatarajiwa kukamilika baadae mwaka huu.