BIdadi ya watu waliofariki dunia kutokana na mafuriko yaliyokuwa yakiambatana na maporomoko ya udongo nchini Brazil imefikia 52.
Serikali ya nchi hiyo imetangaza hali ya tahadhari katika maeneo kadhaa nchini humo kutokana na mafuriko hayo, huku watu wengine zaidi ya 40,000 wakilazimika kuyahama makazi yao kwa usalama baada ya nyumba zao kuharibiwa na mafuriko.
Serikali imesema maporomoko ya udongo yamekuwa ni hatari kubwa kwa watu wanaokaa chini ya milima, kwani mara kadhaa matope yamekuwa yakifunika makazi yao.
Watabiri wa hali ya hewa wanasema nchi hiyo ya Amerika Kusini itarajie mvua zaidi katika kipindi cha saa 24 zijapo.