Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu amemtaka kila mtumishi katika ofisi ya makamu wa rais atimize wajibu wake katika kuleta maendeleo ya Taifa letu.
Ameyasema hayo leo mara baada ya kuwasili rasmi katika ofisi hiyo katika Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma na kupokewa na menejimenti na watumishi na ofisi hiyo.
Akizungumza na watumishi wa ofisi yake Waziri Zungu amewataka wote kufanya kazi kwa ushirikiano na kuahidi kuendelea kusimamia sheria, taratibu na kanuni zilizopo, huku akitoa rai kwa watanzania kuwa chachu ya mabadiliko katika kuhifadhi na kusimamia Mazingira.
“Simamieni sheria bila kumuonea mtu, pale ambapo sheria imekataza jambo simamieni sheria na kuchukua hatua kwa wote wanaokiuka,” amesisitiza.
Awali aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ambae sasa ni wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amekabidhi ofisi rasmi kwa Waziri Zungu na kumtakia kila la heri katika kutekeleza majukumu yake mapya.
“Tumefanikiwa katika katazo la mifuko ya plastiki, tumeridhia mikataba na itifaki mbalimbali na pia tuna programu maalumu ya upandaji mti nchi nzima ambayo ni endelevu,” Simbachawene akimueleza Zungu.
Mbali na mafanikio hayo Waziri Simbachawene amesema elimu inapaswa kutolewa kwa wananchi kuhusu tofauti ya vifungushio na vibebeo ambavyo bado wananchi wanachanganya.
Waziri Zungu ameteuliwa hivi karibuni na Rais Dkt. John Magufuli kushika nafasi hiyo baada ya kufanya mabadiliko madogo katika baraza la mawaziri ambapo Simbachawene aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.