Kondakta wa basi wa kike nchini Kenya ameelezea namna alivyovuliwa nguo na kubaki uchi akiwa katika kituo cha polisi nchini humo ili waweze kuthibitisha jinsia yake.
Theresia Mumbi amesema kuwa alikamatwa na askari polisi wa usalama barabarani na kuweka katika chumba na wanawake wengine, lakini baadae askari walimuamuru kuvua nguo kisha wakamkagua kwakuwa ana ndevu.
“Sijui waliona nini, lakini baada ya hapo waliniamuru kurudi kwenye chumba nilichokuwepo,” amesema Mumbi.
Amesema licha ya kuwa tukio hilo lilitokea Julai 2018 baada ya kukamatwa kuhusiana na nyaraka za utambulisho, bado jambo hilo limo kwenye kichwa chake kama vile limetokea siku za karibuni.
Kutokana na tukio hilo Mumbi amekuwa wakili wa kutetea wanawake wenye utofauti na sasa ameamua kusimulia stori yake ili kukuza uelewa na kuwatia moyo kuzungumza mara wanapokumbana na manyanyaso.
Amebainisha kuwa ana tatizo la homoni kutokuwa na uwiano (hormonal imbalance) jambo lililochangia kuota ndevu. Wakati akiwa mdogo alikuwa akinyoa ndevu hizo lakini baada ya muda aliacha kutokana na ngozi yake kuharibika.
“Ndevu zikawa kubwa, nikaanza kujificha watu wasinione, nikawa natoka kwenda dukani nyakati za usiku pekee,” ameeleza Mumbi.
Kutokana na ugumu wa maisha aliamua kuwa kondakta wa basi ili aweze kujikimu. Wakati akiwa anatekeleza majukumu yake huwatia moyo wanawake wenye changamoto mbalimbali ambao hukutana nao.
Kwa sasa ni mjumbe wa chama cha wanawake wenye ndevu nchini Kenya, na katika mikutano yao huzungumza na kuwatia moyo wanawake hasa walio wadogo.