Mavunde: Vijana washirikishwe kwenye mikakati ya mapambano dhidi ya VVU

0
248

Naibu Waziri wa Kazi,Vijana na Ajira Anthony Mavunde ameitaka Tume ya Kupambana na Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na wadau mbalimbali wa masuala ya VVU na UKIMWI kuwahusisha Vijana katika kupanga mbinu za kukabiliana na ongezeko la maambukizi mapya ya VVU kwa kundi la Vijana ambapo kwa miaka ya hivi karibuni inaonesha kundi kubwa la Vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 limeathirika zaidi ambapo zaidi ya 40% ya maambukizi mapya yanawagusa Vijana katika kundi hilo.

Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akitihimisha mdahalo uliohusisha wanafunzi wa Vyuo Vya Elimu ya Juu na Elimu ya Kati kuhusu mbinu mpya za kupambana na maambukizi mapya kwa Vijana, ambapo amesisitiza ushiriki wa Vijana katika kila mikakati ya kusaidia kutatua changamoto hiyo kwa Vijana ambapo kwa sasa takribani watu 200 wanapata maambukizi mapya kwa siku na 80 wakiwa ni Vijana huku 63 wakiwa ni wasichana.

“Njia hii ya majadiliano ya kuwahusisha Vijana kwenye mambo yanayowahusu wao na maslahi yao ndio njia sahihi,Vijana wapewe nafasi kutoa mapendekezo na mbinu sahihi za kutatua tatizo hili la maambukizi mapya kwa Vijana kwa kuwa wanajua zaidi mazingira yao kuliko mtu mwingine.
Tuondokane na utaratibu wa kuwaamuria vijana katika mambo muhimu pasipo ushiriki wao” Mavunde

Akitoa Maelezo ya awali,Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dr. Leonard Maboko amebainisha mikakati mipya ya kuwafikia Vijana kupitia matamasha ya Burudani ambapo hutumia fursa hiyo kutoa Elimu kwa Vijana kuhusu kujikinga na maambukizi ya VVU na pia kupata muda katika vipindi vya masomo Chuoni kutoa elimu kwa Vijana.