Mazungumzo ya kisiasa kutatua mgogoro Libya

0
350

Mkuu wa Kamisheni ya umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na Mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo Josep Borrell wamesema njia pekee ya kutatua mgogoro wa Libya ni mazungumzo ya kisiasa.

Viongozi hao wametoa tamko hilo mara baada ya kumalizika mkutano wa amani uliofanyika mjini Berlin Ujerumani na kusema kuwa, njia bora ya kutatua mgogoro wa Libya ni mazungumzo ya kisiasa na kusisitiza kuwa wananchi wa Libya ndio wenye haki ya kukubaliana kusimamisha vita, kutatua masuala yao na kudumisha amani.

Mkutano wa kutatua mgogoro wa Libya ulifanyika hapo juzi ukiwashirikisha wawakilishi kutoka nchi 12 na taasisi nne za kimataifa ikiwemo Umoja wa Umataifa, Umoja wa Afrika AU, Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Katika mkutano huo Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amebainisha kuwa washiriki wa mkutano huo wamesisitizia kuheshimiwa kwa vikwazo vya silaha dhidi ya Libya na kutoziunga mkono kijeshi pande hasimu nchini humo.

Hata hivyo saa chache tu baada ya mkutano huo, wanamgambo wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya wanaoongozwa na jenerali Khalifa Haftar wamezishambulia ngome za Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kusini mwa mji mkuu Tripoli.

Picha kuu: Europian Union External Action