Tumieni changamoto kwenye maeneo yenu kujiajiri- Dkt Ngugulile

0
413


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile amewataka wanawake na vijana nchini kutumia changamoto zilizopo katika maeneo yao kama fursa ya kujiajiri na kuajiri watu wengine.

Dkt. Ndugulile ameyasema hayo wilayani Ludewa mkoani Njombe wakati alipotembelea vikundi kazi vya wanawake na vijana vinavyojishughulisha na kutengeneza barabara na madaraja madogo wilayani humo.

“Sijawahi kuona kitu kama hiki tangu nianze ziara zangu katika mikoa na wilaya, hongereni, mmethubutu na mkaamua kutumia fursa hii kujiajiri, huu ni mwanzo mzuri na mtafika mbali,” amesisitiza Dkt. Ndugulile.

Ameongeza kuwa jambo linalofanywa na vikundi vya wanawake na vijana mkoani humo linaendana moja kwa moja na dhana ya maendeleo ya jamii ya wananchi kushiriki katika shughuli za kimaendeleo katika maeneo yao.

“Jambo hili mnalofanya ni jambo jema la msingi litawasaidia kupata kipato na kujiinua kiuchumi kwani serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt Magufuli inasisitiza watu kufanya kazi hasa vijana na wanawake,” amehitimisha Dkt. Ndugulile huku akizitaka halmashauri nyingine kuiga mfano na kuwashawishi wanawake na vijana kujiunga kwenye vikundi vya kijasiriamali.