Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imesema kuwa inaendelea na zoezi la usajili na utambuzi wa watu, uzalishaji wa namba za utambulishi wa taifa na vitambulisho na ugawaji wake kwa wananchi ili waweze kuvitumia kusajili kadi (laini ) za simu kwa alama za vidole na huduma nyingine.
Katika kurahisisha upatikanaji wa namba za utambulisho wa taifa, NIDA imebuni njia mbalimbali zitakazowasaidia wananchi kupata namba zao na kupunguza msongamano mkubwa katika ofisi zao.
Njia hizo ni kwenda kuchukua namba katika ofisi za vijiji husika ambazo zitakazopelekwa na NIDA, kutumia USSD *152*00# na kufuata maelekezo, au kutuma ujumbe mfupi wa simu kwenda namba 15096.
Mwombaji anapochagua kutumia njia ya kutuma ujumbe mfupi atatakiwa kuandika jina la kwanza na jina la mwisho, tarehe ya kuzaliwa, jina la kwanza la mama, na jina la mwisho la mama. Huduma hii ni bure.
Aidha, wananchi wanaweza kupata namba na vitambulisho vyao katika ofisi za NIDA au vituo vya muda vya mamlaka hiyo vilivyo karibu nao.
Hadi Januari 15, NIDA ilikuwa imezalisha idadi kubwa ya namba za utambulisho wa taifa ambapo kati ya hizo namba za utambulisho 6,806,096 hazijatumika kusajili laini za simu kwa alama za vidole.
Mamlaka hiyo imewasihi wananchi ambao tayari wamepata namba kuzitumia kusajili laini zao ili wasifungiwe ifikapo Januari 20, mwaka huu kwani sio lazima kuwa na kitambulisho ndipo uweze kusajili.