SIMANZI: Mfanyakazi akutwa ameuawa ofisini

0
451

Mfanyakazi wa Shirika la Transparency International (TI) Kenya, amekutwa ameuawa katika ofisi hizo jana, Januari 15.

Mwili wa aliyekuwa mfanya usafi wa shirika la TI linaloshughulika na mapambano dhidi ya rushwa lenye ofisi zake Kisumu umekutwa ukiwa chini huku damu zikiwa zimetapakaa katika moja ya vyumba vya ofisi hiyo alipokuwa akiishi.

Inasemekana kuwa mauaji ya marehemu Caren Adhola (45) yalitokea usiku wa kuamkia jana, ambapo yalitekelezwa na watu wasiofahamika.

“Caren amekuwa mfanyakazi wetu kwa miaka sita. Hakuwa na kesi yoyote na hajawahi kutoa malalamiko ya vitisho juu ya maisha yake,” amesema Mkurugezi wa TI-Kenya, Titus Ogala wakati akizungumza na Daily Nation.

Mwili wa Adhola ulichukuliwa na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga, na tayari uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini wahusika.

Picha kuu: wananchi waliokusanyika katika ofisi za TI- Kenya yalipotokea mauaji ya Caren Adhola.  Picha: Nation Media Group