Jeshi la Polisi nchini Tanzania limefanikiwa kupunguza ajali za barabarani kwa asilimia 69.4 ndani ya kipindi cha miaka minne kutoka Novemba 2015 hadi sasa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, SACP David A. Misime kuanzia Novemba 2015 kurudi nyumba kwa kipindi cha miaka minne ajali zilikuwa 73,871.
Wakati hali ikiwa hivyo kuanzia Novemba 2015 hadi Septemba 2019 ajali zilikuwa 22,621 ikiwa ni sawa na upungufu wa 51,850 (asilimia 69.4).
SACP Misime amesema kuwa mafanikio hayo yametokana na mikakati iliyowekwa na Jeshi la Polisi, taasisi nyingine za serikali na wadau mbalimbali.
Mbali na hayo mambo mengine yaliyochangia kupungua kwa ajali ni mfumo wa matumizi ya VTS, udhibiti wa mwendo kasi katika vituo mbalimbali vilivyopo katika barabara mbalimbali kwa kutumia spidi rada, kuwatoza faini madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani na baadhi yao kfungiwa leseni zao za udereva.
Kufanikiwa kupunguza ajali za barabarani ni tafsiri kuwa vifo vilivyokuwa vikitokana na ajali za barabarani, idadi ya waliokuwa wakipata ulemavu na uharibifu wa mali umepungua.